Picha kutoka: BBC
21 Apr 2022 Toleo la habari Uchunguzi wa mazingira

David Attenborough atuzwa tuzo la Umoja wa Mataifa la ngazi ya juu zaidi

Picha kutoka: BBC

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) lilitangaza leo kuwa Hababi David Attenborough ndiye mshindi wa Tuzo la Mabingwa wa Dunia la Mafanikio ya Kudumu  kutokana na juhudi zake za utafiti, uandaji wa makala, na uhamasishaji kuhusu utunzaji na uboreshaji wa mazingira. 

"Hababi David Attenborough amejitolea katika maisha yake kurekodi hadithi ya upendo uliopo kati ya wanadamu na mazingira, na kuitangaza kwa ulimwengu.  Iwapo tutaweza kukabiliana na hali mbaya ya hewa na uharibifu wa bayoanuai na kusafisha mifumo ya ekolojia iliyochafuliwa, hili litatokea tu kwa sababu baadhi yetu kwa mamilioni tulianza kupenda sayari ambayo alituonyesha kwenye televisheni," Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP alisema.  “Kazi ya Hababi David itaendelea kuhamasisha watu wa umri wowote kutunza mazingira na kuwa kizazi cha uboreshaji.”

Kazi ya Attenborough kama mtangazaji, mwanahistoria wa asili, mwandishi, na mhamasishaji wa mazingira imedumu kwa zaidi ya miongo saba.  Anajulikana zaidi kwa kazi yake katika Kitengo cha Historia ya Asili cha BBC, ikijumuisha makala kama vile Life on Earth, the Living Planet, Our Planet and Our Blue Planet.  Kwa kuongezea, uhamasishaji wake wa kuhifadhi na kuboresha bayoanuai, kutumia nishati jadidifu, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ya kukuza matumizi ya lishe kutoka kwa mimea huchangia kufikiwa kwa mengi ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

"Ulimwengu unapaswa kushirikiana.  Matatizo haya hayawezi kutatuliwa na taifa moja - haijalishi ukubwa wa taifa hilo.  Tunajua matatizo ni yepi na tunajua jinsi ya kuyatatua.  Tunachokosa ni ushirikiano wa kuyashughulikia, "Attenborough alisema alipopokea Tuzo la Mafanikio ya Kudumu.   “Miaka 50 iliyopita, nyangumi walikuwa karibu kutoweka kote ulimwenguni.  Kisha watu wakashirikiana na kwa sasa kuna nyangumi wengi zaidi baharini kuliko ilivyowahi kushuhudiwa na wanadamu. Tukichukua hatua kwa pamoja, tunaweza kutatua matatizo haya.”    

Attenborough amekuwa mfuasi wa muda mrefu na shupavu wa ushirikiano wa kimataifa kuhusiana na mazingira.  Katika mwaka wa 1982, wakati wa  mkutano wa 10 wa Baraza Linaloongoza UNEP, aliambia Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa: “Kile ambacho wewe na mimi na watu wengine wa kawaida kote ulimwenguni tunaweza kufanya hakitaokoa ulimwengu asilia. Maamuzi makuu, majanga makubwa yanayotukabili, yanaweza tu kushughulikiwa na serikali na ndiyo sababu shirika hili ni muhimu sana.”

Tuzo hiii la Mafanikio ya Kudumu linatolewa katika mwaka wa kihistoria kwa jumuiya ya kimataifa ya mazingira. Mwaka wa 2022 ni maadhimisho ya miaka hamsini tangu kutokea kwa Kongamano la Umoja wa Mataifa la mwaka wa 1972 kuhusu Mazingira ya Binadamumjini Stockholm, Uswidi, ambalo lilikuwa mojawapo ya mikutano ya kwanza ya kimataifa kuhusu mazingira. Kongamano hilo lilichochea uundaji wa wizara na mashirika ya mazingira kote duniani, lilianzisha mikataba mipya ya kimataifa ya kushirikiana kutunza mazingira, na kupelekea kuundwa kwa UNEP, ambayo inaadhimisha miaka 50 mwaka huu.   

Washindi wa awali ni pamoja na mhamasishaji wa mazingira Robert Bullard (2020), mtetezi wa haki za mazingira na asili Joan Carling (2018) na mwanabayolojia wa mimea José Sarukhán Kermez (2016).  Washindi huchaguliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, ambaye pia hutoa tuzo hilo.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu  Tuzo la UNEP la Mabingwa wa Dunia
Tuzo la Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa la Mabingwa wa Dunia hutuza watu binafsi, makundi na mashirika ambayo huchukua hatua za kusababisha mabadiliko chanya kwa mazingira.  Tuzo linalotolewa mara moja kwa mwaka la Mabingwa wa Dunia ni tuzo la umoja wa mataifa la ngazi ya juu linalotolewa kwa heshima ya mazingira.   Hutuzwa kwa viongozi wa kipekee kutoka kwa serikali, mashirika ya uraia na sekta binafsi.

Kuhusu Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia

Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia 2021-2030 ni wito wa kutunza nakuboresha mifumo ya ekolojia kote ulimwenguni kwa manufaa ya binadamu na sayari. Unalenga kusitisha uharibifu wa mifumo ya ekolojia, na kuiboresha ili kufikia malengo ya kimataifa. Baraza la Umoja wa Mataifa lilitangaza Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia unaongozwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa ikijumuisha kuimarisha juhudi za wanasiasa za kuiboresha pamoja na maelfu ya miradi inayoendelea.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.  

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Keishamaza Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa
Moses Osani, Afisa wa Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa