24 Feb 2020 Toleo la habari Uchumi usiochafua mazingira

Kukuza biashara zisizochafua mazingira na uchumi endelevu barani Afrika

Kampala, Februari 24, 2020: Waunda sera na wadau kote barani Afrika wanakusanyika ili kujadili uwezekano wa kuwa na uchumi unaotumia nishati isiyochafua mazingira kwenye sekta ya kilimo chini ya Programu ya 'Switch Africa Green'. Jukwa hili la Kukuza Biashara Zisizochafua Mazingira na Uchumi Endelevu Barani Afrika huandaliwa na Shirika La Mazingira la Umoja wa Mataifa na Wizara ya Maji na Mazingira ya Uganda.

Jukwaa la kikanda la kukuza biashara zisizochafua mazingira na uchumi endelevu ni njia mwafaka ya kukuza chumi zisizochafua mazingira, kuhakisha urudufushaji na kuimarisha biashara zisizochafua mazingira barani Afrika. Ni kutokana na uelewa huu ndiyo mkutano utakaojiri mjini Kampala uganda tarehe 24 na 25 februari utajadili namna na mbinu za kukuza uchumi endelevu na kuimarisha biashara zisizochafua mazingira barani Afrika.

“Programu ya 'Switch Africa Green' tayari inapendekeza mbinu endelevu, ikiwa ni pamoja na teknolojia ya nishati ya samadi; kushughulikia taka kwa njia ya elektroniki, kufanya kilimo kwa kutumia mbinu za kiasili, kuwa na viwanda visivyotumia nishati ya kuchafua mazingira na kuwa na viwanda na kampuni nyingi kwenye eneo moja. Pia, kuwa na hoteli za kiwango cha juu na kadhalika," alisema Frank Turyatunga, Naibu Mkurugenzi wa UNEP wa Ofisi ya Afrika. "Ni muhimu kutumia elimu na maarifa kutoka nchi mbalimbali kubuni sera zinazoweza kutumiwa kwingi ili kuhakikisha matokeo chanya na utekelezaji kikamilifu katika ngazi ya kitaifa.”

Jukwaa hili linaleta pamoja viongozi kutoka nchi wanachama wafadhili wa 'SWITCH Africa Green' ikijumuisha Burkina Faso, Ethiopia, Ghana, Kenya, Mauritius, Afrika Kusini na Uganda kwa ushirikiano na wadau wengine wanaoshiriki katika ukuzaji wa uchumi unaotumia nishati isiyochafua mazingira kama vile waunda sera, mashirika ya biashara, sekta ya binafsi, taasisi za fedha, taasisi za uchumi za kikanda, mashirika ya maendeleo na mashirika ya uraia.

"Kukabiliana na changamoto zinazoyakabili mazingira kunahitaji kutumia fursa zilizopo kama vile kukuza uchumi usiochafua mazingira ili kuleta maendeleo endelevu na kupata manufaa mengi kama vile kutunza mazingira, kuimarisha uchumi na kubuni nafasi za kazi. Vitu muhimu vinavyoweza kusaidia kuleta mabadiliko kama vile uwekezaji kwa nishati isiyochafua mazingira, kuweka sera na sheria, uhamasishaji, kushirikiana, kufungua biashara zinazotumia ubunifu wa kutochafua mazingira," alisema Tom Okurut, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kushughulikia Mazingira nchini Uganda.

Jukwaa la 'SWITCH Africa Green' linalenga kubuni fursa kutokana na changamoto za mazingira kutokana na uelewa kuwa kukuza uchumi usiochafua mazingira ni nguzo ya maendeleo endelevu. Pia kuna manufaa anuai ya kutunza mazingira kama vile kuimarisha uchumi, kubuni nafasi za kazi, kupunguza umaskini, manufaa anuai ya kiuchumi na kuleta mapato. Programu hii hujishughulisha sanasana na vitu muhimu vinavyoweza kusaidia kuleta mabadiliko kama vile uwekezaji kwa nishati isiyochafua mazingira, kuweka sera na sheria, kubuni bidhaa vinavyoweza kutumiwa zaidi ya mara moja, uhamasishaji na mafunzo ya ujasiriamali unaojali mazingira, kufungua biashara zinazotumia ubunifu kutochafua mazingira. 

"Makubaliano Mapya Kuhusu Maendeleo Ulaya)- hasa jinsi EU inavyoshughulikia Ajenda 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa-inalenga kuleta mabadiliko kwa kasi kwa kusisitiza kuwepo na sera za maendeleo jumuishi kama vile nishati endelevu, hatua za kushughulikia mazingira zinazojumuisha uwekezaji na biashara, ajira, usawa wa kijinsia, vijana, uongozi mzuri, demokrasia, uzingatiaji wa sheria na wa haki za binadamu, uhamiaji na uhamaji," alisema Pavlos Evangelidis, msimamizi  mkuu wa ubalozi wa Muungano wa Ulaya nchini Uganda.

Tangu kuzinduliwa kwake mwaka wa 2014, 'Switch Africa Green' ni jukwaa ambalo limechukua usukani wa nchi saba barani Afrika ili kuziwezesha kuzalisha na kutimia bidhaa kwa njia endelevu huku zikikuza na kuimarisha uchumi. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, programu hii imefaulu kutoa mafunzo kwa kampuni ndogondogo mno, kampuni ndogo za biashara na kwa kampuni za wastani (MSMEs). Pia limeandaa programu za majaribio na za kukuza ujuzi wa kuzalisha na kutumia bidhaa kwa njia endelevu.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Switch Africa Green

Programu ya SWITCH Africa Green husaidia nchi saba za Burkina Faso, Ethiopia, Ghana, Kenya, Mauritius, Afrika Kusini na Uganda kuwa na maendeleo endelevu kupitia kuleta mabadiliko yatakayowezesha  kukuza uchumi unaotumia nishati isiyochafua mazingira  kupitia uzalishaji na matumizi ya bidhaa kwa njia endelevu. Linalenga kubuni fursa kutokana na changamoto za mazingira kutokana na uelewa kuwa kukuza uchumi usiochafua mazingira ni nguzo ya maendeleo endelevu. Pia kuna manufaa anuai ya kutunza mazingira kama vile kuimarisha uchumi, kubuni nafasi za kazi, kupunguza umaskini, manufaa anuai ya kiuchumi na kuleta mapato. Programu hii hujishughulisha sanasana na vitu muhimu vinavyoweza kusaidia kuleta mabadiliko kama vile uwekezaji kwa nishati isiyochafua mazingira, kuweka sera na sheria, kubuni bidhaa vinavyoweza kutumiwa zaidi ya mara moja, uhamasishaji na mafunzo ya ujasiriamali unaojali mazingira, kufungua biashara zinazotumia ubunifu kutochafua mazingira. 

SWITCH Africa Green ilianzishwa na kufadhiliwa na Kamisheni ya Ulaya na inatekelezwa na UNEP. Wafadhili wa mradi huu ni taasisi za Umoja wa Mataifa, hasa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) naUNOPS, One Planet network na African Roundtable on SCP (ARSCP). Wabia wakuu kutoka kwa serikali ni kama vile wizara husika (Mazingira, Viwanda, Kilimo, Utalii, Uchumi na Fedha na zile za Kitaifa za Kutunza Mazingira/Mashirika ya Usimamiaji/Mamlaka za Usimamiaji).

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP in mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo. UNEP hufanya kazi pamoja na serikali, sekta ya kibinafsi, mashirika ya uraia na taasis zinginezo za Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa kote ulimwenguni.

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Mohamed Atani, Afisa wa Mawasiliano ya Ukanda, Ofisi ya Afrika, UNEP:  Simu: +254 727531253