18 Feb 2020 Tukio Misitu

Miti ni uhai

Bustani za miche kubwa, ndogo au zisizonawiri, zinazopatikana barani Afrika hutofautiana kutokana na jinsi zinavyotengenezwa, zinavyohifadhiwa na kiwango cha ubora wake. Baadhi zinamilikiwa na serikali, baadhi zinamilikiwa na mashirika yasiyokuwa ya kibiashara na zingine zinamilikiwa na wakulima binafsi.

Edward Lutawo Phiri, kutoka Zambia, na babake ni wakulima wa sampuli hii, na bustani walioshirikiana kuanzisha ni maarufu mno katika nyanja ya biashara. Alipokuwa mtoto mdogo, Lutawo Phiri aliona babake akipanda miche na kufurahishwa. Babake alipoaga, Lutawo Phiri aliendeleza kazi hii na kuimarisha bustani hiyo hadi sasa anaajiri watu 12 na imefikia hekta 3.

Kwa kweli, alibahatika kwa sababu babake alikuwa na shamba kubwa lililokuwa na chanzo cha kudumu cha maji. Lina mabonde kidogo, maji ya kutosha na mchanga wenye rutuba. Alitandaza eneo hilo na kuinua mchanga, ili kutengeza bustani jinsi alivyotaka na kuinua kwa kutumia fito za kudumu. Pia, alitumia mchanga na mawe madogomadogo kusaidia mizizi kupenyeza na kusaidia maji kupita. Ana aina ya mchanga kutoka msituni unaotunza unyevunyevu na kuhifadhi rutuba.

Pia, yeye hupanda na kupandikiza miti ya matunda. Kupandikiza ni jinzi ya upandaji unaohusisha kuunganisha vitu viwili tofauti, hasa mashina mawili ya mimea tofauti. Mara nyingi, mashina ndiyo hupandikizwa. Sehemu ya juu hujulikana kama kitawishina na sehemu ya chini au mzizi hujulikana kama shina au mizizishina. Kitawishina na mizizishina ni sharti vitoke kwa aina moja ya mimea au kwa mimea ya jamii moja.

Kupandikiza inamaanisha kuwa mimea bora miwili inaunganishwa na kuwa mmea mmoja. Kitawishina huwa na tumba moja au zaidi ambapo matawi yatachipuka na kuzalisha matunda baadaye. Njia zote ambazo hutumiwa kuunganisha mimea hujulikana kama kupandikiza, lakini kitawishina kikiwa tu na tumba moja, hujulikana kama kutumbisha.

Miti ya matunda ambayo hupandikizwa zaidi nchini Zambia ni miembe, miparachichi na miti ya jamii ya machungwa.

image

"Baada ya kupandikiza, mimi huipanda msimo wa mvua. Hupanda pamoja na maharagwe na njugu kwa sababu haviathiri umeaji wa miti," anasema Lutawo Phiri. "Mimi pia hufanya kilimo cha misitu na ninakuza miche ya kiasili kwa ajili ya kutengeneza mbao kama vile mkangazi mwekundi ambo huchukua miaka saba kabla ya kuwa tayari."

"Tusitegemee tu mmea mmoja," anasema "Tunapaswa kupanda miti kwa sababu inatusaidia kukabiliana na mafuriko na kiangazi na kutupa dawa za kukabiliana na magonjwa. Pia hutupa mvua. Miti ni uhai."

Ijapokuwa kuna bustani zinazokabiliwa na ukosefu wa maji, Lutawo Phiri anaeleza kuwa kwa kutunza misitu vizuri, kwa kuzuia mioto ya misituni na kutokata miti kiholelaholea vimemsaidia kudumisha kuwepo kwa maji na ahitaji kuchimba visima virefu.

Ili kuzuia wadudu vamizi na magonjwa, Lutawo Phiri hutumia matawi ya mwarobaini anayobondabonda na kuchanganya na maji na kisha kunyunyuzia miche yake. Kutengeneza mbolea, yeye hutumia matawi na kuchanganya na samadi. Huchanganya na mchanga ili kuongeza rutuba mchangani.

David Ngwenyama, Meneja wa mkoa wa Mradi wa Zambia wa Bustani za Misitu anasema kuwa ananuia kufanya kazi na Lutawo Phiri kwa sababu ni mwaminifu, ana aina bora zaidi ya miche na huwa tayari kutoa ushauri na kusaidia inapohitajika.

Lutawo Phiri alituzwa Medali ya Dhahabu kwa huduma za kupekee na rais mstaafu wa Zambia Michael Sata. 

image

Kwa mjibu wa Judith Walcott, mtaalamu wa masuala ya utunzaji wa bustani wa Kituo cha Ufuatiliaji na Kuhifadhi cha Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, "Wakati ambapoMradi wa UN-REDD  unapoendelea kusaidia nchi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia masuluhisho ya kiasili, na lengo la kutunza na kuhifadhi misitu, kazi kama zile zinazofanywa na Lutawo Phiri ni muhimu mno. Matumizi ya miche bora zaidi na miche ya kiasili ni muhimu mno ili kuboresha misitu na kupata manufaa mengine zaidi kutokana na misitu. Manufaa hayo ni kama vile kuhifadhi bayoanuai na mifumo mingineyo ya ekolojia.

 

Masuluhisho kutokana na mazingira  ni njia mwafaka ya kuboresha maisha ya binadamu, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kutunza sayari yetu tunayoiahi ndani. Ijapokuwa mazingira yanakabiliwa na changamoto, kutokana na kuangamia kwa viumbe mara 1000 zaidi kuliko katika kipindi kingine chochote kwenye historia, aina milioni moja huangamia. Mbali na umuhimu wa kufanya uamuzi, ikiwa ni pamoja na COP 15 kuhusu bayoanuai, mwaka wa 2020 unaofahamika kama "mwaka mkuu" ni fursa mwafaka ya kuokoa mazingira. Hatima ya mazingira inategemea hatua tutakazochukua sasa.

 

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ingrid Dierckxsens.