Mioto misituni
23 Feb 2022 Toleo la habari Nature Action

Visa vya Mioto Misituni Kuongezeka kwa asilimia 50 kufikia mwaka wa 2100 ila Serikali Hazijajiandaa, Wataalam Waonya

  • Hata eneo la Akitiki, ambalo hapo awali halikushuhudia hali hii, limo hatarini kukumbwa na mioto mibaya zaidi, wataalam wanasema, kabla ya Mkutano wa Baraza la Mazingira mjini Nairobi.
  • Mioto misituni na mabadiliko ya tabianchi "hushirikiana kudhuru"
  • Wito unatolewa kwa serikali kubadilisha kwa kiasi kikubwa uwekezaji wa Mioto misituni ili kulenga kuizuia na kujitayarisha

Nairobi, Februari 23, 2022 - Mabadiliko ya tabianchi na mabadiliko ya matumizi ya ardhi yanakadiriwa kupelekea visa vya mara kwa mara vya mioto mibaya zaidi misituni, na ongezeko la kimataifa la mioto mikali zaidi wa asilimia 14 kufikia mwaka wa 2030, asilimia 30 kufikia mwishoni mwa mwaka wa 2050 na asilimia 50 kufikia mwishoni mwa karne hii, kwa mjibu wa ripoti mpya ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na GRID-Arendal.

Wito unatolewa kwa serikali kubadilisha zinavyotumia fedha kushughulikia mioto misituni, kwa kubadilisha uwekezaji kutoka kwa kuishughulikia na kukabiliana nayo hadi kwa kuizuia na kujitayarisha. 

Ripoti hiyo, Kusambaa kama Mioto Mwituni: Tishio Kubwa kwa Mazingira Kutokana na Mioto Mibaya Zaidi, inaonyesha kuwa hatari inaongezeka hata kwa Akitiki na maeneo mengine ambayo hapo awali hayakushuhudia mioto misituni.  Ripoti hiyo imetolewa kabla ya wawakilishi wa mataifa 193 kukutana Nairobi kwa kikao cha 5 cha Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA-5.2), kati ya Februari 28 na Machi 2, 2022.

Chapisho hilo linatoa wito kwa serikali kupitisha ‘Mfumo Mpya wa Kujiandaa kwa Mioto,’ huku thuluthi mbili ya pesa za matumizi zikitengewa upangaji, kuzuia, kujiimarisha, na thuluthi moja ikitengewa kuishughulikia. Hivi sasa, ushughulikiaji wa moja kwa moja wa mioto misituni kwa kawaida hupokea zaidi ya nusu ya pesa za matumizi yanayohusiana na ushughulikiaji, huku upangaji na uzuiaji ukipokea chini ya asilimia moja.

Ili kuzuia mioto, waandishi wanatoa wito wa mchanganyiko wa data na mifumo ya ufuatiliaji inayozingatia sayansi na maarifa ya kiasili na ushirikiano thabiti wa kikanda na kimataifa.

Ushughulikiaji wa serikali kwa sasa kwa mioto misituni mara nyingi hufuja pesa. Wale wafanyakazi wa huduma ya dharura na wazima moto walio mstari mbele wanaohatarisha maisha yao kupambana na mioto mibaya misituni wanahitaji kusaidiwa,” alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP.  Tunapaswa kupunguza uwezekano wa kutokea kwa mioto mibaya misituni kwa kujiandaa vyema: kuwekeza zaidi katika kupunguza ewezekano wa mioto kutokea, kushirikiana na wenyeji, na kuimarisha ahadi za kimataifa za kupambana na mabadiliko ya tabianchi."

Mioto misituni huathiri vibaya mataifa maskini zaidi duniani.  Madhara huendelea kwa siku, majuma na hata kwa miaka baada ya mioto kupungua, hali iliyo kukizingiti kwa kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa na kupanua pengo la ukosefu wa usawa katika jamii:

  • Afya ya watu huathiriwa moja kwa moja kwa kuvuta moshi wa mioto ya misituni, na kusababisha matatizo ya kupumua na magonjwa ya moyo na kuongezeka kwa madhara ya afya kwa walio hatarini kuathiriwa zaidi; 
  • Gharama za kukuza uchumi baada ya mikasa ya mioto misituni kwenye maeneo yaliyoathiriwa na mioto misituni zinaweza kuzidi uwezo wa nchi za kipato cha chini;
  • Maeneo ya maji huharibiwa na vichafuzi kutoka kwa mioto misituni; pia inaweza kusababisha mmomonyoko wa udongo na kuathiri vyanzo vya maji;
  • Taka zilizobaki mara nyingi husababisha uchafuzi sana na zinahitaji kutupwa ipasavyo. 

Mioto misituni na mabadiliko ya tabianchi hushirikiana kudhuru.  Mioto misituni huwa mibaya zaidi kwa kuchombewa na mabadiliko ya tabianchi kutokana na kuongezeka kwa ukame, joto la juu hewani, unyevu wa chini kiasi, radi, na upepo mkali, hali inayopelekea misimu ya mioto mikali kwa kipindi kirefu wakati wa kiangazi.  Wakati uo huo, mabadiliko ya tabianchi huzidishwa na mioto misituni, hasa kwa kuharibu mifumo muhimu ya ekolojia na iliyo muhimu kwa kaboni kama vile maeneo ya mboji na misitu ya mvua.  Hali hii huathiri mazingira na kuifanya kuwa vigumu kukomesha joto linalozidi kuongezeka.

Wanyamapori na makazi yake ya kiasili huwa hawaepuki mioto misituni, hali inayopelekea baadhi ya wanyama na mimea kuwa karibu kuangamia.  Mfano wa hivi majuzi ni mioto misituni nchini Australia katika mwaka wa 2020, inakayokadiriwa kuangamiza mabilioni ya wanyama wa kufugwa na wa mwituni.  

Ni muhimu kuelewa vyema mienendo ya mioto misituni. Kufikia na kudumisha usimamizi wa ardhi na wa mioto kutegemea eneo kunahitaji sera mbalimbali, mfumo wa kisheria na matuzo ili kuchochea matumizi mwafaka ya ardhi na mioto.

Uboreshaji wa mifumo ya ekolojia ni njia muhimu ya kupunguza uwezekano wa kutokea kwa mioto misituni kabla haijatokea na kujiimarisha baada ya kutokea kwake. Urejeshaji wa maeneo oevu na urejeshaji wa spishi kama vile buku, urejeshaji wa maeneo ya mboji, kujenga mbali na mimea na kuhifadhi maeneo wazi ni baadhi ya mifano ya uwekezaji muhimu wa kuzuia, kujiandaa na kujiimarisha.

Ripoti hiyo inahitimisha kwa kutoa wito wa kuwepo kwa viwango dhabiti vya kimataifa kwa usalama na afya ya wazima moto na kupunguza hatari wanazokabiliana nazo kabla, wakati na baada ya kuishughulikia.  Hii ni pamoja na kuhamasisha kuhusu hatari za kuvuta moshi, kupunguza uwezekano wa kutishia maisha, na kuwawezesha wazima moto kuwa na maji ya kutosha, chakula cha kutosha, kupumzika na kuhisi vyema kabla ya kupokezana zamu.   

Ripoti hiyo ilitolewa ili kuunga mkono UNREDD na Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia. . UNEP itakuwa inachunguza jinsi uwekezaji zaidi unavyoweza kufanywa ili kupunguza hatari za mioto kwa mifumo muhimu ya ekolojia kote ulimwenguni.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu GRID-Arendal

GRID-Arendal ni kituo cha mawasiliano kuhusu mazingira kisicho cha kibiashara kilicho na makao yake nchini Norwe.  Tunafanyia data ya mazingira kazi kuwa vifaa bunifu vya habari, kutokana na sayansi na kutoa huduma za kujenga uwezo zinazowezesha usimamizi bora wa mazingira.  Tunalenga kufahamisha na kuelimilisha hadhira ya kimataifa na kuchochea wafanya maamuzi kuleta mabadiliko chanya.  GRID-Arendal inashirikiana na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa na washirika wengine kote duniani.

Kuhusu Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia  

Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia 2021-2030 unatoa wito wa kutunzwa na kuboreshwa kwa mifumo ya ekolojia kote ulimwenguni, kwa manufaa ya watu na mazingira.   Unalenga kukomesha uharibifu wa mifumo ya ekolojia, na kuiboresha ili kufikia malengo ya kimataifa.  Baraza la Umoja wa Mataifa lilitangaza Muongo wa Umoja wa Mataifa na unaongozwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa.      Muongo wa Umoja wa Mataifa unaunda vuguvugu dhabiti lenye msingi mpana wa kimataifa ili kuimarisha uboreshaji na kuiwezesha dunia kuwa na hatima endelevu.   Hiyo itajumuisha kuimarisha uwezo wa kisiasa wa uborejeshaji na maelfu ya miradi inayoendelea. 

UNEP@50: Wakati wa kutafakari kuhusu yaliyopita na kutazamia yajayo

Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira ya Binadamu mjini Stockholm, Uswidi katika mwaka wa 1972, ulikuwa mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kutumia neno "mazingira" kwenye anwani yake kwa mara ya kwanza. Kuanzishwa kwa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) ni mojawapo wa matokeo makuu ya kongamano hili lilianzisha mambo mengi.   UNEP ilianzishwa kuwa kitengo cha kushughulikia mazingira cha Umoja wa mataifa kote ulimwenguni.  Shughuli zitakazoendelea katika mwaka wa 2022 zitaangazia hatua zilizopigwa na yatakayojiri katika miongo ijayo. 

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani.  Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.  

Kwa mawasiliano zaidi, tafadhali wasiliana na: Keisha Rukikaire, +254 722 677747,

Keisha Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa